Press Contact

SISU News Center, Office of Communications and Public Affairs

Tel : +86 (21) 3537 2378

Baruapepe : news@shisu.edu.cn

Anuani :550 Dalian Road (W), Shanghai 200083, China

Soma Zaidi

Uchunguzi wa Mabavu ya Ushindani wa Serikali ya Tanzania katika Tukio la CMG


28 May 2022 | By 斯瓦希里语(sw) | SISU

3. Uhakiki na Maelezo

3.1 Usimamizi na Kanuni za Vyombo vya Habari

Vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika utendakazi wa demokrasia. Wakati wa uchaguzi, kazi ya jukumu lake la usimamizi linadhihirika katika kukagua na kujadiliana kwa wagombea, serikali, sera za vyama, matokeo ya uchaguzi na ufanisi wa mashirika ya usimamizi wa uchaguzi. Ufuatiliaji baada ya uchaguzi ni muhimu vilevile. Vyombo vya habari vinaweza kufahamisha umma utendakazi wao katika uchaguzi na kusaidia umma kuwawajibisha wale walio madarakani baada ya uchaguzi.

Kwa hivyo, vyombo vya habari ni muhimu kwa demokrasia. Ikiwa vyombo vya habari havingekuwepo, mchakato wa uchaguzi haungeweza kuwa wa haki na wa kuaminika. Uchaguzi huru na wa haki hauhusishi tu uhuru wa kupiga kura na ujuzi wa jinsi ya kupiga kura, bali unashirikisha pia mchakato ambapo wapiga kura hushiriki katika mijadala ya hadhara na kufahamu kikamilifu vyama vya siasa, sera, wagombea na mchakato wenyewe wa uchaguzi ili kufanya maamuzi sahihi.

Vyombo vya habari ni mfuatiliaji muhimu wa uchaguzi wa kidemokrasia kwa kuhakikisha uwazi wa mchakato wa uchaguzi. Kutokuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari ni kinyume na utaratibu wa uchaguzi wa kidemokrasia wenyewe.

3.1.1 Mipaka isiyo dhahiri ya usimamizi wa vyombo vya habari 

Japo maofisa wa TCRA walifanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu kusitishwa kwa CMG, haikuweka hati rasmi juu ya tukio hilo kwenye tovuti. Msemaji wa TCRA  alieleza kuwa  CMG ilikiuka Kanuni za Huduma za Utangazaji (Utangazaji wa Uchaguzi wa Vyama vya Siasa) za 2020, ambayo ilikuwa na utata. 

Kifungu cha 16 cha kanuni kinaandika kwamba:

"As they become available, special care shall be taken to ensure the accuracy of all results broadcast." (The Political Party Elections Broadcasts Code 13)

 

 “Matokeo ya uchaguzi kadri yanavyopatikana, uangalifu maalum uchukuliwe ili kuhakikisha usahihi wa matokeo yote yanayotangazwa." (Tafsiri yangu)

 

Watangazaji na waundaji wa makala katika mtandao waliombwa kufuata kanuni hii, ambayo ni pamoja na kuzingatia kanuni na taratibu za usimamizi wa vyombo vya habari vya Tanzania ili kuhakikisha kuwa habari zinazochapishwa kuhusu uchaguzi za vyama vya siasa ni za kweli, za haki na zenye uwiano, lakini hazisemi wazi adhabu kwa wanaokiuka. Adhabu hizo ambazo hazieleweki zinamaanisha kuwa CCM inaweza kutafsiri kanuni kwa maslahi ya vyama vya siasa na hivyo kusababisha uwanja usio wa haki katika uchaguzi.

Katika tarehe 23, Juni, mwaka 2020, Idara ya Habari ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliifuta leseni ya gazeti la Tanzania Daima kwa madai kuwa limekiuka sheria ya habari na maadili ya uandishi wa habari mara kadhaa. Blogu Rasmi ya Serikali ilichapisha uamuzi huo wa adhabu. Lakini katika waraka rasmi "Kusitisha Leseni ya Kuchapisha na Kusambaza Gazeti la Tanzania Daima", ukiukaji huo ulielezwa kwa ufupi kuwa "ukaidi, ubishi, dharau kwa Mamlaka" za nchi, na wakati fulani nia dhahiri." Ukweli ni kuwa mwenyehisa wa gazeti hilo ni mke wa mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe.

Majukumu ya TCRA pia hayana mipaka dhahiri. TCRA inasimamia vyombo vya habari, huku hailindi uhuru wa vyombo vya habari. Katika tukio la Machi 17, 2017 ambapo viongozi wa mkoa walikatisha utangazaji wa vipindi vya CMG, maofisa wa TCRA hawakufanya lolote. Afisa aliyehojiwa na MCT alisema, mamlaka hiyo ni chombo cha Serikali kinachojitegemea, chenye jukumu la kusimamia sekta za mawasiliano ya posta na Utangazaji nchini Tanzania. Ilianzishwa chini ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania Na.12 ya mwaka 2003 ili kudhibiti mawasiliano ya kielektroniki, huduma za posta na usimamizi wa masafa ya taifa. "Iwapo kituo chochote cha utangazaji kimevamiwa, uvamizi wa kituo cha utangazaji ni kosa la jinai, na ni suala la polisi." Kwa mujibu wa maofisa wa TCRA(MCT Report 20).

3.1.2 Udhibiti Uliobana Vyombo vya Habari Kabla ya Uchaguzi

Tanzania ina misingi ya kisheria ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari. Ibara ya 39 (2) ya Katiba inahakikisha uhuru wa kujieleza. Hili pia linathibitishwa na Kifungu cha 53(1) cha Sheria ya Uchaguzi, kinachovilazimu vyombo vya umma vya utangazaji; redio, televisheni na magazeti kuhakikisha wagombea wa vyama vya siasa wanapewa fursa ya muda wa kutoa sauti wakati wa kampeni.

Sheria inawaruhusu wagombea wa urais, makamu wa rais na vyama vyote vya kisiasa kutumia huduma za utangazaji za redio na televisheni wakati wa kipindi rasmi cha kampeni. Inahimiza kutopendelea hata kidogo na inakataza vyombo vya serikali vya habari visibague mgombeaji yeyote katika utangazaji wa habari na katika kutolewa kwa nafasi kwa wagombeaji. NEC ina wajibu wa kuratibu matumizi ya vyombo vya habari ili kuhakikisha usawa huo kwa wagombea na vyama vyao.

Lakini, chini ya marekebisho mapya yaliyotolewa hivi karibuni, nafasi ya utendaji ya vyombo vya habari na mashirika ya kiraia imepunguzwa. Hivyo, uhuru na demokrasia imepunguzwa nguvu. Tarehe 10, Agosti, 2020, TCRA ilifanyia Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta marekebisho (Maudhui ya Utangazaji wa Redio na Televisheni) 2020 ili kuongeza kifungu kipya katika Kifungu cha 37: Watangazaji wa nchini ambao tayari wamepewa leseni ya kufanya kazi lazima wapate kibali kutoka kwa mdhibiti ili kutangaza maudhui ya kitaifa au kimataifa. Aidha, watangazaji wa ndani wakishirikiana na watangazaji wa nje wawajibike kisheria.

Sababu ya haraka ya marekebisho ya sheria hiyo ni Radio Free Afrika (RFA) kutangaza mahojiano yenye utata na Tundu Lissu. Tarehe 10 Agosti 2020, TCRA iliwaita viongozi wa RFA na kuwafungulia mashtaka ya kukiuka kifungu cha 15(2) (b), (c) na 16 cha Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) za 2018.

Kwa mujibu wa hukumu kwenye tovuti ya TCRA, kipindi cha “Amka na BBC” cha RFA kilimhoji Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. Lissu alisema kuwa alitaka kumuenzi aliyekuwa rais mstaafu Benjamin Mkapa, lakini serikali ilimkataza.

 “Inasikitisha sana, tumefika kwa wakati tulioambiwa kwa mujibu wa ratiba. Kutuambia kwamba hatuwezi kuingia uwanjani kwa sababu tumechelewa tuliona ilikuwa ni namna tu ya kusema kwamba hawataki tushiriki kumuaga huyu aliyekuwa Rais wetu.... Haiwezekani tena kama hutakiwi na waandaaji wa msiba ukilazimisha kwenda watakwambia wewe ndo mchawi. Sisi hatutaki kuonekana ni wachawi wa mzee Mkapa, tumesema waendelee tu Mungu awabariki.” (TCRA 2)

TCRA inaamini kwamba RFA haikuthibitisha ukweli wa maneno ya Tundu Lissu. Ilitangaza maudhui yenye upendeleo bila kupata ufafanuzi kutoka kwa msemaji wa serikali. Kwa njia hiyo, RFA ilikiuka kanuni na maadili ya vyombo vya habari. TCRA ikawahoji viongozi wa RFA na ikawaamuru wawasilishe maandishi yaliyohusu maelezo yao juu ya kosa lao (2-4).

Lakini katika kazi ya vyombo vya habari, ukweli ni kuwa, ni vigumu sana kwa waandishi wa habari kuhakikisha uwiano kamili na inachukua muda mwingi na pesa nyingi kufikia ukweli kamili. Katika hali nyingi zaidi, utangazaji wa habari hubadilika, na wanahabari wakitoa ripoti za ufuatiliaji wanapokusanya ushahidi mpya.

Kwa wale wanaofanya kazi katika nyanja za vyombo vya habari, matendo ya TCRA ni makali hata kupindukia. Ili kuzuia usambazaji wa habari zenye lawama, waandishi wa habari wa kigeni sasa wanatakiwa kuandamana na karani wa serikali. a TCRA hayakuharibu maendeleo ya vyombo vya habari vya Tanzania tu bali pia yanawaletea wananchi mashaka kuhusu nia na motisha za TCRA. Katika tukio la Paul Makonda, aliomba watangazaji watangaze filamu ambayo haikuwa na uwiano wa nyenzo kutoka pande mbili kwa sababu hazikuwepo sauti ya upande wa pili katika filamu hiyo na TCRA ikaufumbia macho mwendo huo usiofaa. Wakati vyombo vya habari viliporipoti maslahi ya vyama, TCRA ilianza kuvituhumu vyombo vya habari kwa kupuuza uwiano kati ya ukweli wa habari. Mfumo wa kisheria kwa upana una msingi wa kutosha wa kuendesha chaguzi wa kidemokrasia, lakini utekelezaji wake unaonekana ulitumiwa kwa njia zisizo sawa kwa washikadau mbalimbali wakati wa uchaguzi mkuu wa 2020.

Katika mfumo wa utawala wa kiimla, bunge ama halipo au linadhibitiwa na chama tawala. Migogoro mikubwa kati ya serikali na bunge hutokea pia. Katika utawala wa mabavu, bunge ni dhaifu katika madaraka yake, lakini  bado linaweza kuwa kitovu cha shughuli za vyama vya upinzani. Wakati wa marekebisho ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Redio na Televisheni), vyama vya upinzani bado viliweza kutoa maoni yao, hivyo kuthibitisha kuwa bado kuna "ushindani wa kutunga sheria" kati ya chama tawala na vya upinzani nchini Tanzania. Nadhani hiki ndicho kinachotofautisha siasa za Tanzania na utawala wa kiimla.

3.2 NEC: Taasisi ya Uchaguzi Imedhibitiwa na Chama Tawala

Utendakazi mzuri wa mifumo ya uchaguzi unahitaji taasisi zinazojumuisha, endelevu, zisizo na upendeleo na huru. Taasisi ya uchaguzi inahitaji kuwa inakubalika kwa kutekeleza kanuni, na kuhakikisha uchaguzi ni wa haki kwa ushirikiano wa vyama vya siasa na wananchi (Elklit na Reynolds 93).

Uchaguzi ni kipengele muhimu cha kutofautisha utawala wa mabavu ya ushindani kutoka kwa utawala wa kiimla na utawala mwingine wa kimabavu. Katika tawala za kiimla na tawala zingine za kimabavu, uchaguzi wa kidemokrasia ama haupo au hauna ushindani. Kinyume cha hayo, katika tawala za kimabavu, uchaguzi wa kidemokrasia ndiyo njia pekee ya kuhalalisha mamlaka na ushindani wa vyama vingi unaonyesha mwelekeo mdogo wa ushindani.

Katika tukio la kusimamishwa kwa CMG, vyombo vya habari viliadhibiwa kwa kuchapisha matokeo ya uchaguzi katika baadhi ya majimbo bila kibali cha NEC. Kama taasisi ya usimamizi wa uchaguzi Tanzania Bara, NEC inakabiliwa na matatizo mawili: mashaka juu ya uhuru wake na ukosefu wa kuaminiwa na wananchi.

3.2.1 Mashaka ya Umma Juu ya Uhuru wa NEC

Shirika la Afrika wa Uchaguzi, Demokrasia na Utawala (ACEDG) umeweka kigezo cha kutathmini uhuru wa Taasisi Zinazoendesha Uchaguzi (Election Management Bodies,  EMBs  kwa ufupisho) za Afrika, ikiwa ni pamoja na:

 

(a) The independence of EMBs should be secured constitutionally, and their budget should be voted directly by the legislative bodies responsible for allocation of budgets.

(b) The African Union in consultation with EMBs should work towards the adoption of common standard norms for the management of elections in Africa.

(c) EMBs should conduct themselves with integrity, independence, transparency, and impartiality.

(d) EMBs must independently appoint their secretariat.

(e) Each election management body should structure a process that allows for public scrutiny of all processes (ACEDG Conference) 

 

a) Uhuru wa EMBs unapaswa kuhakikishwa kikatiba na bajeti yake ipigiwe kura moja kwa moja na bunge;

b) EMBs zinapaswa kuwa na muundo rasmi katika vyombo mbalimbali vya kanda ndogo na ndani ya Umoja wa Afrika 

c) EMBs zitafanya kazi kwa uadilifu, uhuru, uwazi na bila upendeleo;

d) EMBs zitateua katibu wake zenyewe;

e) EMBs itatekeleza mfumo mmoja ambapo michakato yote itaruhusu usimamizi wa umma.  (Tafsiri yangu)

 

Kama mwamuzi mkuu wa uchaguzi, Taasisi ya usimamizi wa uchaguzi inapaswa kuwa huru katika uchaguzi. Kwa Tanzania Bara, NEC ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kikatiba ya kusimamia uchaguzi. Ilianzishwa mwaka 1993 na imesimamia uchaguzi mkuu tangu wakati huo. Katika kipindi hiki, Tanzania imeshuhudia mijadala mikubwa kuhusu suala la uhuru wa NEC.

NEC imekabidhiwa na katiba majukumu ya kuandikisha wapiga kura, kuteua wagombea, kuandaa uchaguzi na kusoma matokeo ya uchaguzi. Katiba inaitaja Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ni idara inayojitegemea ambayo, katika kutekeleza majukumu yake, hailazimiki kutii amri au maagizo ya mtu au idara yoyote ya serikali, au maoni ya chama chochote cha siasa. Aidha, mahakama hazina mamlaka ya kuchunguza mwenendo wowote wa NEC katika utendaji wa kazi zake kwa mujibu wa Katiba.

Hata hivyo, wajumbe wa NEC wanateuliwa na kuondolewa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Kamati ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO) iliwahi kuhoji iwapo NEC inafanya kazi ikiwa uhuru: kwanza, uteuzi wa wajumbe wa NEC huteuliwa na rais aliyepo, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala. Pili, kwa sababu rais anaweza kutengua uteuzi, wajumbe wa NEC hawana muda maalum. Tatu, katiba na sheria ya uchaguzi haitengi chanzo cha fedha kwa NEC. Nne, NEC haina watumishi wake katika ngazi ya wilaya na jimbo. Badala yake, inategemea wafanyakazi wa serikali za mitaa ambao wengi wao ni makada wa CCM.

Kwa kuzingatia muundo, ufadhili na uhusiano wa mikoa na CCM, NEC haiwezi kuonekana kama chombo huru cha uchaguzi.

3.2.2 Kutoaminika na umma

Utafiti wa Makulilo unathibitisha kutokuwa na imani na NEC kwa wananchi wa upinzani. Washiriki wa upinzani waliohojiwa walitoa sababu zifuatazo: Rais anateua wajumbe wa NEC moja kwa moja, lakini pia ni mwenyekiti wa chama tawala na pia anashiriki katika uchaguzi mkuu, kwa hivyo, yeye huwa na upendeleo wakati wa kuteua wajumbe. Wanachama wanapatikana vivyo hivyo wakati wa kutekeleza majukumu. (Makulilo 96)

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalendo, Seif Sharif Hamad, alibainisha kuwa NEC haikuwa mshiriki bila upendeleo katika mchakato wa uchaguzi mkuu: 

 

"The current electoral commission does not guarantee independent elections, as it favours the ruling party since its chairman and some leaders. They are appointed by the president, who is the leader of the ruling party." (nukuu ktk. Makulilo 2012: 102)

 

“Tume ya sasa ya uchaguzi haitoi dhamana ya uchaguzi huru, kwani inapendelea chama tawala tangu mwenyekiti na baadhi ya viongozi. Wanateuliwa na rais ambaye ndiye kiongozi wa chama tawala.”(Tafsiri yangu)

 

Sambamba na hayo, wananchi nao wanaonyesha mashaka juu ya uhuru wa NEC. Katika utafiti wa Ngware, ni asilimia 1.6 tu ya waliohojiwa waliamini kuwa kamati hiyo ilikuwa huru, asilimia 36 waliamini kuwa kamati hiyo ilikuwa na wajumbe wa chama tawala bila uwakilishi kutoka chama cha upinzani. Katika utafiti huo huo, asilimia 53 ya waliohojiwa waliomba uchunguzi juu ya uadilifu wa mwenyekiti wa kamati, muda wake wa kazi na kama anapaswa kuteuliwa mwenyekiti; 33% walionyesha wasiwasi kwa masuala ya fedha na usimamizi wa kamati (Ngware et al. 2002: 68). 

Kwa mtazamo huo, wananchi na vyama vyote vya upinzani vimetilia shaka juu ya  uhuru wa NEC, ambao umepunguza uaminifu wa taasisi hiyo. Hii imethibitishwa na utafiti wa Bakari na Mushi, ambao walitaja kuwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1995 na 2000 nchini Tanzania ulitiliwa shaka sana na washiriki, na si kwa sababu wanachama wa vyama vya upinzani walikataa kukubali kushindwa, bali kwa sababu hapakuwa na makubaliano kuhusu matokeo( Bakari na Mushi 41).

Imekuwa bayana kwamba, kwa kiasi kikubwa, NEC siyo taasisi huru ya inayosimamia uchaguzi. Ina uhusiano na rais na chama tawala cha Tanzania, hata ikapoteza uaminifu wa umma na uhuru wake kutiliwa shaka na vyama vya upinzani.. 

3.3 Matumizi ya Mamlaka ya Utendaji Kupindukia 

Katika matukio mawili yaliyoelezwa katika sura ya pili, inaonekana kuwa vyombo vya kukomesha vurugu vya serikali vilishiriki. Matumizi ya kupita kiasi ya vyombo vya kukomesha vurugu vya serikali hayaingilii uendeshaji wa kawaida wa vyombo vya habari tu, bali pia yanakandamiza uwezo wa upinzani kwa kiasi wakati wa uchaguzi mkuu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofuata mfumo wa utawala wa rais, ambapo rais ndiye mwenye jukumu la kumteua mtendaji mkuu. Rais wa Tanzania ni mkuu wa nchi, amiri jeshi mkuu. Katika kutekeleza madaraka ya amiri jeshi mkuu, rais wa Tanzania anaweza kuelekeza majeshi kufanya operesheni maalum ndani ya nchi. Wakati huo, kwa mujibu wa Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (CURT 1977), Rais wa Tanzania anaweza kuteua viongozi wakuu ambao ni pamoja na makamu wa rais, mawaziri na majaji wa mahakama kuu na mahakama ya rufani ya Tanzania ("CURT"). Viongozi wengine wanaoteuliwa na rais ni pamoja na katibu mkuu, katibu mkuu wa wizara, wakuu wa wilaya, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa wilaya.

Wahudumu hawa wa serikali wanatakiwa kuvitumikia vyama vyote vya siasa katika uchaguzi bila upendeleo. Lakini ukweli ni kwamba wao wamekuwa watumishi wa siasa wala si watumishi wa wananchi, kwa sababu kuteuliwa kwao na rais kunatokana na utiifu wao kwa chama tawala. Hivyo watu hawa hawawezi kukwepa kutenda kwa upendeleo katika kipindi cha kati ya uchaguzi. Wanahamasisha wapiga kura kwa niaba ya chama tawala na kwa njia nyingi tofauti kuwezesha kampeni za wagombea wa chama tawala kwa kutumia rasilimali za serikali (magari, wanausalama n.k.) (TEMCO 2006: 168).

3.3.1 Vyombo vya Serikali Kuingilia Usambazaji wa Taarifa wa Vyombo vya Habari

Katika tukio la kuzimwa kwa CMG tarehe 26, Agosti, mwaka wa 2020, jeshi la polisi la TPF liliweka vikwazo kwa uhuru wa viongozi wa upinzani wakati wa uchaguzi mkuu. Inafamika kuwa, madaraka ya utendaji, yanayoagizwa na rais wakati wa uchaguzi, hayakutumikia vyama vya siasa kwa usawa, angalau si katika matukio ya CMG.

Katika tukio la kuingiliwa kwa kipindi cha CMG, Paul Makonda, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, aliingia studioni na kukatiza utendakazi wa kawaida wa vyombo vya habari na akatumia mamlaka yake kuwatisha watumishi waliokuwepo. Baada ya tukio hilo, alikataa kuomba msamaha. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na MCT, Makonda alifanya hivyo kutoka maslahi na mapendeleo yake, hata aliitaja Shilawadu kama "programu yangu". Hata hivyo, bado inaweza kuonekana kwamba maafisa wa mikoa walioteuliwa na rais wana mamlaka ya kuingilia utendakazi wa kawaida wa vyombo vya habari.

Ingawa Sheria ya Uchaguzi ya 1985 iliomba vyombo vya habari kugawa muda wa maongezi na habari sawa miongoni mwa wagombea na vyama vyote vya siasa ukweli haukuwa hivyo. 

Data ya kihistoria inaonyesha kuwa chama tawala hufurahia sehemu kubwa zaidi ya utangazaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi. Ripoti ya Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) ilioneysha kuwa vituo vya redio vya RTD na STZ vilitengewa muda wa sekunde 105,971 kwa CCM, huku chama cha pili kwa ukubwa cha CUF kikipata sekunde 31,557. Kadhalika, Televisheni Tanzania (TVT) na Televisheni Zanzibar (TVZ) zilitengea CCM sekunde 114,475 za muda wa matangazo, ikifuatiwa na CHADEMA yenye sekunde 22,287 (MISA 2005: 3-4).

Kwa hivyo, si vigumu kukisia kwamba mamlaka ya utendaji ya Tanzania yanaweza kuingilia maudhui yanayotangazwa na vyombo vya habari wakati wa uchaguzi na kuweka kikamilifu ajenda ya sifa kwa wapiga kura, kwa kufichua ripoti nyingi zilizochaguliwa kwa uangalifu.

3.3.2 Mamlaka ya Utendaji ni Shinikizo Kwa Vyama vya Upinzani

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2015, mazingira ya kisiasa nchini Tanzania yalibadilika sana. Mikusanyiko ya watu iliwekewa vikwazo vikali na TPF. Kulingana na habari za BBC, TPF ilipiga marufuku maandamano yote ya upinzani mnamo tarehe 7, Juni, 2020. Tukio hilo limetokea baada ya vyama vya upinzani kutarajia mikusanyiko ingefanyika nchini kote, ili kupinga uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku mijadala kwenye televisheni (BBC "Uchaguzi"). 

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kufuatilia Uchaguzi (IEOM) kutoka Taasisi ya Afrika ya Uchaguzi Endelevu wa Kidemokrasia (ELSA), katika uchaguzi mkuu wa 2020, kampeni za uchaguzi katika maeneo mbalimbali kwa ujumla zilikuwa za amani na tulivu. NEC imesema ilipokea malalamiko 12 na rufaa saba wakati wa kampeni, zote zilitatuliwa ipasavyo. Lakini, IEOM imepokea taarifa kadhaa: vyama vya upinzani vilikandamizwa na nguvu ya utendaji wakati wa kampeni, ikiwamo kufutwa kwa kampeni zilizoidhinishwa awali, kukamatwa na kuwekwa ndani kwa wagombea wakati wa kampeni, TPF kutumia mabomu ya machozi na kuwatawanya wafuasi wa upinzani, kutishwa na kudhibitiwa ("ELSA"). Kulingana na ripoti ya BBC, kabla ya uchaguzi, TPF ilitoa kanuni mpya ambazo zilikataza mikusanyiko ya watu. Kiongozi cha TPF alieleza kuwa katika kipindi cha maombolezi ya kitaifa, vyombo vya kukomesha vurugu vya serikali vihakikisha amani na utulivu (BBC "Uchaguzi"). 

Siku hiyo, Chadema iliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhusu kurejea kwa Tundu Lissu ambaye alikuwa atawasili Tanzania Julai 28 kama mgombea urais wa Chadema. Chadema iliwahimiza wafuasi wake kumkaribisha Lissu, ambapo TPF ilisema uamuzi wa kurejea kwa Lissu ni uhuru wake, lakini bado wataendelea kufuatilia kwa karibu ka mkutano huo una kibali au hauna.

Kama chombo cha kukomesha vurugu cha serikali, TPF inaongozwa moja kwa moja na rais wa Tanzania na inaendeshwa kwa maslahi ya chama ya utawala. Katika uchaguzi mkuu, imekuwa chombo cha chama tawala kukandamiza vyama vya upinzani kwa njia isiyo ya moja kwa moja. 

Katika matukio haya, CCM ilitumia madaraka ya utendaji kwa kupita kiasi ambapo ilidhibiti rasilimali za umma. Iliviomba vyombo vya habari kutoa taarifa zenye upendeleo, iliwatisha wagombea wa vyama vya upinzani na hata iliendesha uchaguzi kwa njia zisizo rasmi kama vile kupeleka polisi kukandamiza upinzani. Hivyo, imekuwa vigumu kwa uhuru na haki ya uchaguzi Tanzania kufikia wastani wa kidemokrasia.

Matukio ya CMG ni mfano mmoja wa mashindano baina ya CCM na vyama vingine vya upinzani kwenye nyanja ya vyombo vya habari: kwanza, vyombo vya kukomesha vurugu vya serikali havikuhudumia vyama vya siasa kwa haki, viliweka vikwazo kwenye uhuru wa viongozi wa upinzani binafsi; pili, vyombo vya habari viliadhibiwa kwa kuchapisha video zinazohusika.

Kanuni za huduma ya utangazaji (maudhui) (matangazo ya uchaguzi wa chama) ni msingi wa adhabu, ambazo mipaka yake si dhahiri. Kwa hiyo, TCRA, ambayo ni chombo cha utendaji kinachodhibitiwa na rais, ina uwezo wa kutafsiri kanuni hizi kwa mujibu wa maslahi ya vyama.

4. Hitimisho

Katika matukio mawili ya CMG, matendo ya CCM yalionyesha mabavu ya ushindani kwa kiasi kikubwa. Kiwango cha uhuru, kiwango cha haki ya uchaguzi, kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari na muundo wa mamlaka ya kisiasa zote ni viashiria vinavyoshutumu utawala wa mabavu ya ushindani. Kwa hiyo, uchaguzi wa kidemokrasia nchini Tanzania unatofautiana na utawala wa mabavu na utawala wa chama kimoja. Misingi ya  kisheria  na kuwepo kwa vyombo huru vya habari, imevipa vyama vya upinzani fursa ya kushindana na chama tawala. Ingawa inawezekana kwa upinzani kuchukua utawala kupitia kwa mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia, ni vigumu kuuchukua. 

Kwa sababu ya muundo wa mamlaka Tanzania, ukuu wa urais unafungamana na mamlaka ya utendaji na hivyo kwa kiasi fulani rais na chama tawala wana uwezo wa kuingilia sheria na kuweka kanuni za mchakato wa uchaguzi. Kutokana na hali hii, kuna tofauti kubwa sana kati ya chama tawala na vyama vya upinzani katika uwezo wa kupata rasilimali katika mashindano ya uchaguzi. Kwa mtazamo wa sheria ya vyombo vya habari, utaratibu wa uchaguzi, na mamlaka ya kiutawala, mazingira ya uchaguzi wa kidemokrasia nchini Tanzania haiwezi kuitwa haki. Ni dhahiri kwamba CCM ina uwezekano mkubwa wa ushindi katika uchaguzi na uwezekano huu umekuwa ukipanuka kwa sababu ya uwezo wake wa kupata rasilimali katika nyanja mbalimbali. Inawezekana kwamba siku moja mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia utakuwa njia ya CCM kutafuta uhalali wa kisiasa, la sivyo demokrasia itapoteza maana yake katika nchi hii.

 

Marejeleo

Africa Conference on Elections, Democracy and Governance (ACEDG). “Conference Held 7–10 April, Pretoria.” N.p., 2006.< www.elections.org.za/africaconference >.(tar.2.Feb.2022)

“CURT 1977 (The Constituion of the United Republic of Tanzania).” Rsf.Org. N.p., 1977.< https://rsf.org/sites/default/files/constitution.pdf > . (tar.1.Feb.2022)

“Application No. 5 of 2019 Media Council of Tanzania & Others v The Attorney General of the United Republic of Tanzania.” East African Court of Justice. N.p., 2019. Web. (tar.8.Jan.2022)

Bakari, Mohamed L., and Samwel S. Mushi. Prerequisites for Democratic Consolidation in Tanzania.” Democratic Transition in East Africa. N.p., 2005. Google Scholar. Web. (tar.18.Jan.2022)

“Bulldozing’ the Media.” Reporters Without Borders. N.p., 2020. Web. (tar.9.Jan.2022)

Elklit, J, and A Reynolds. “The Impact of Election Administration on the Legitimacy of Emerging Democracies: A New Comparative Politics Research Agenda.” Commonwealth & Comparative Politic 40 (2010): 86–119. Google Scholar. Web. (tar.20.Jan.2022)

“EISA Election Observation Mission to the 2020 General Elections in Tanzania.” Elsa.Org. N.p., 2020.< https://www.eisa.org/pdf/tan2020preliminary.pdf >..(tar.1.Feb.2022)

Linz, Juan. An Authoritarian Regime: Spain. Tidnings och Tryckeri Aktiebolag, 1963. Google Scholar. Web. (tar.14.Jan.2022)

---. Totalitarian and Authoritarian Regimes. Handbook of Political Science. Google Scholar. Web. 1975. (tar.14.Jan.2022)

Levitsky, Steven, and Lucan Way. “Elections Without Democracy: The Rise of Competitive Authoritarianism.” Journal of Democracy 13 (2002): 51–65. Project Muse. Web. (tar.18.Jan.2022)

---. “Beyond Patronage: Ruling Party Cohesion and Authoritarian Stability.” APSA 2010 Annual Meeting (2010): 1–46. Google Scholar. Web. (tar.18.Jan.2022)

Makulilo, Alexander B. “Unleveled Playfield and Democracy in Tanzania.” Journal of Politics and Law 5.2 (2012): 96–106. Google Scholar. Web. (tar.18.Jan.2022)

Morse, Yonantan L. “Party Matters: The Institutional Origins of Competitive Hegemony in Tanzania.” Democratization 21 (2013): 655–677. Google Scholar. Web. (tar.16.Jan.2022)

Ndamungu, Omari Issa. “THE TRIPARTITE POWERS OF THE EXECUTIVE ORGAN OF STATE IN TANZANIA.” IJSSMR 3 (2013): 74–87. Google Scholar. Web. (tar.18.Jan.2022)

Ngware, Suleiman, and Ocharo. Prerequisites for Democratic Consolidation in Tanzania. Aarare: Tema Publication Company Ltd., 2002. Google Scholar. Web. (tar.1.Feb.2022)

Paget, Dan. “Tanzania: Shrinking Space and Opposition Protest.” Journal of Democracy 28 (2017): 153–167. Google Scholar. Web. (tar.16.Jan.2022)

Paget, Dan. “Tanzania: The Authoritarian Landslide.” Journal of Democracy 32 (2021): 61–76. Google Scholar. Web. (tar.15.Jan.2022)

“Probe Report on the Invasion of Clouds TV Studios.” Media Council of Tanzania. N.p., 2019.< Https://Mct.or.Tz/Wp-Content >.(tar.20.Jan.2022)

Schedler, Andreas. “Elections Without Democracy: The Menu of Manipulation.” Journal of Democracy 13 (2002): 36–50. 

“Tanzanian Authorities Ban Radio and TV Station.” Zimbabwe Chapter of the Media Institute of Southern Africa. N.p., 2020.< https://zimbabwe.misa.org/2020/08/28/tanzanian-authorities-ban-radio-and-tv-station/>. (tar.20.Jan.2022)

“Tanzania Leader’s aside on ‘Limits’ of Freedom Raises Fears.” International Press Institute. N.p., 2017.< https://ipi.media/tanzania-leaders-aside-on-limits-of-freedom-raises-fears/>. (tar.4.Feb.2022)

“Tanzania Gags Another Media Outlet, Demands Apology for Seven Days.” The Standard. N.p., 2020.. (tar.4.Feb.2022)

TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania). “WITO NA MASHATKA YA UKIUAJI WA KANUNI ZA MAWASILIANO YA KIELEKTRONIKI NA POSTA (MAUDHUI YA UTANGAZAJI WA REDIO NA TELEVISHENI), 2018 DHIDI YA RADIO FREE AFRICA.” RSF. N.p., 2020.< https://rsf.org/sites >. (tar.20.Jan.2022)

TEMCO (Tanzania Election Monitoring Committee). “The Report of the 1995 General Elections in Tanzania.” temco. N.p., 1997.< http://www.temco.udsm.ac.tz/index.php/publications/reports >. (tar.4.Feb.2022)

---. “The Report of the 2005 General Elections in Tanzania, Dar Es Salaam: University of Dar Es Salaam.” temco. N.p., 2006.< http://www.temco.udsm.ac.tz/index.php/publications/reports >. (tar.4.Feb.2022)

“Uchaguzi Tanzania 2020: Polisi Wapiga Marufuku Mikusanyiko Ya Kumpokea Lissu.” BBC. N.p., 2020 . (tar.2.Mar.2022)

Gawanya:

Press Contact

SISU News Center, Office of Communications and Public Affairs

Tel : +86 (21) 3537 2378

Baruapepe : news@shisu.edu.cn

Anuani :550 Dalian Road (W), Shanghai 200083, China

Soma Zaidi