Wito
WITO MKUU WA SISU
Wito mkuu wa SISU ni ‘格高志远, 学贯中外’ (Gé gāozhì yuǎn, xué guàn zhōngwài). Kwa Kiingereza wito huu umefasiriwa kuwa “Integrity, Vision and Academic Excellence.” Kwa Kiswahili, twaweza kuufupisha wito huu kuwa, “Uadilifu, uaminifu, maono ya hekima na elimu pana” kwa kuzingatia chanzo na nia za SISU.
“格高志远gāozhì yuan” kutoka The Book of Rites ni matini msingi katika maandishi ya Confucius (Kǒngzǐ) ambapo Bwana anasema kuwa “Wale walio waaminifu kwa maneno na waadilifu kwa vitendo wataweza kuishi na maono bora ya hekima na wafe na sifa nadhifu”. Chanzo kingine kinapatikana katika Wen Xuan, (Selections of Refined Literature), iliyohaririwa na Xiao Tong wa Nasaba ya utawala wa Liang ya Kusini (502-557). Hapo inasema: “Kwa uaminifu na maono yenye hekima, mtu anaonekana kama hashindiki.”
Sehemu ya pili ya kifungu cha wito ni, “学 贯 中外 - Xué guàn zhōngwài”, tunayoifasiri kama, “Usijifunzie nyumbani peke yako.” Sehemu hii ya kifungu inapendekeza mtazamo linganishi wa tamaduni za China na za nje ili kukuza mawasiliano duniani.
Hivi basi, wito huu unalenga kufikia ubora wa elimu inayoleta China pamoja na dunia. Hivi ndivyo SISU inavyojitoa kufikia lengo lake la kuuwasilisha ulimwengu China na kuiwasilisha China kote ulimwenguni, huku ikitilia tofauti za tamaduni maanani.
WIMBO WA SISU
Wimbo wa SISU (Ode to SISU) ulitangazwa rasmi na Kamati ya Uongozi wa Chuo Kikuu Machi 27, 1989 baada ya kutathminiwa na wataalam kadha akiwemo Lu Zaiyi kutoka Shanghai Conservatory of Music. Uliandikwa na Zhuang Kairen, mhitimu wa PhD kutoka Idara ya Kiingereza ya chuo kikuu. Nao muziki ulioandaliwa na Wang Zhihui, mwanafunzi wa 1985 wa shahada ya kwanza ya Biashara za Kimataifa. Mwaka 2009 wakati SISU ilipoadhimisha miaka 60. Maneno ya wimbo yalilinganishwa na wito mpya mkuu.