Historia kwa Muhtasari

1949-1950

Shule ya Kirusi ya Shanghai

Misingi ya Jamhuri ya Wananchi China, ilipokuwa ikianzilishwa, mahitaji makubwa ya wataalamu wa Kirusi ambao wangesaidia katika ujenzi wa usoshalisti kutoka Muungano wa kale wa Kisovieti walihitajika. Kwa mujibu wa pendekezo la meya wa Shanghai wa wakati huo, Chen Yi, Halmashauri ya Mashariki ya China ya Kamati Kuu ya Chama (CPC) na Kamati ya Manispaa ya Shanghai ya CPC, paliamuliwa pawe na shule ya Kirusi Shanghai ikiwa ni mshiriki wa awamu ya nne ya Chuo Kikuu cha Mapinduzi cha Mashariki ya China. Na basi mnamo Desemba 1949 shule ilianzishwa ikiwa ni shule ya kwanza ya lugha ya kigeni ya Jamhuri ya Wananchi China (PRC).

Shule hiyo changa ya Kirusi ilikuwa ya mkondo mmoja kitaaluma. Ilijishughulisha na masomo ya Kirusi kama lugha na fasihi kutoka mataifa ya Kisovieti tu. Wahitimu wake walihudumu katika nyanja za utafsiri, ufasiri, ukalimani na ualimu wa Kirusi.

1950-1952

Chuo cha Lugha za Kigeni Shanghai

Mnamo 1950, ili kukidhi mahitaji ya China ya wataalamu katika diplomasia na biashara ya kimataifa, palianzishwa masomo ya Kiingereza Shanghai na shule ikabadili jina na kuwa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni Shanghai kikiwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Mapinduzi ya Wananchi Mashariki ya China. Chuo hicho kilihamishiwa katika Barabara ya Tiyuhui Mashariki (mahali ambapo tawi la chuo kikuu cha Jinan kilipokuwa). Hapa ndipo mahali ambapo tawi la Hongkou la SISU lilipo sasa. Mwezi wa nne 1951, Idara ya Lugha za Asia ulianzishwa na kuanza kutoa mafunzo ya Kiburma, Kivietnam na Kiindonesia. Tangu mwezi wa nane 1952, Chuo cha Lugha za Kigeni Shanghai ni chuo kikamilifu, kwa wakati wa mwanzo kikitoa mafunzo kuhusu lugha 5, nazo ni Kirusi, Kiingereza, Kiburma, Kivietinamu na Kiindonesia.

1952-1956

Chuo Kikuu cha Kirusi

Kuanzia muhula wa pili wa mwaka 1952, mfumo wa kitaifa wa usajili katika vyuo ulizinduliwa na Wizara ya Elimu ikafanya mabadiliko katika vyuo vyote vya elimu ya juu vya China. Hii ilimaanisha kuwa, Idara ya Lugha na Fasihi za Asia ya Chuo cha Lugha za Kigeni Shanghai zilihamishiwa Chuo Kikuu cha Peking na Septemba 1952 chuo kikapewa jina jipya la Chuo Kikuu cha Kirusi Shanghai (Shanghai Russian College) na kuanza mafunzo ya shahada ya miaka mitatu. Mwaka uo huo, kundi la kwanza la wataalamu wa Kisovieti walianza kufanya kazi chuoni na wakapewa jukumu la kuelekeza mpangilio wa mfumo wa mafunzo na utunzi wa vitabu vya kusomeshea Kirusi - maandishi yake na mazungumzo.

Katika kipindi hicho mfumo wa kufundisha ulibadilika kutoka elimu ya kitaaluma na ukawa wa mafunzo ya kazi maalum. Dhana ya elimu ilipangwa upya; hivi kwamba, katika kitivo kilichoandaliwa upya, ile iliyokuwa sehemu kina ya mafunzo na utafiti iliondolewa na badala yake pakaja vikundi kumi vya kufunza na kufanya utafiti wenye malengo maalum. Baadhi ya yaliyolengwa ni kufunza mazoea ya kazi, kutafsiri, historia ya fasihi na pia isimu na lugha. Mipangilio mipya ya masomo kama vile mfumo mpya wa uongozi wa wanachuo zilianzishwa na zikafanikiwa.

1956-1994

Taasisi ya Lugha za Kigeni Shanghai

Baada ya kuidhinishwa na Halmashauri ya Serikali mwaka 1956, chuo hiki kikuu kilipata jina jipya rasmi la Taasisi ya Lugha za Kigeni Shanghai (Shanghai Foreign Language Institute). Mabadiliko haya yalikuja pamoja na vitivo kubadilishwa na kuongezeka; hapo basi kukaja vitivo vya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani nayo elimu ikawa ya shahada ya kwanza inayotolewa kwa muda wa miaka 4. Septemba 12, 1963, chuo hiki kikuu kiliorodheshwa na serikali kuu kama chuo kikuu cha kitaifa chini ya Wizara ya Elimu.

Tangu miaka ya sabini, baada ya kupitishwa kwa Sera ya Marekebisho na Kufungua Nchi, China imeshuhudia kupanuka kwa kazi za kidiplomasia na mawasiliano ya kimataifa, hivyo basi kuongezeka kwa mahitaji ya utaalamu wa lugha za kigeni. Mwaka 1982, chuo kilianza kubadilisha kuongeza kutoka mkondo mmoja wa masomo ya lugha na kuundwa kiwe chuo kinacholenga miseto ya matakwa ya mahitaji ya lugha za kigeni kitaifa. Kwa sababu hii, masomo mapya yamekuwa yakiongezwa tangu 1983.

Wakati uo huo, chuo kimekuwa kikifanya uboreshaji na uimarishaji wa mifumo yake ya elimu na usimamizi wa mafunzo. Septemba 1983, chuo kilipata kibali (kutoka kwa Kamati ya Serikali ya Shahada za Kitaaluma za Vyuo) cha kutoa shahada ya uzamifu PhD (daktari) katika Kiingereza na Kirusi. Mwaka 1993, kwa uongozi wa Tume ya Elimu ya Nchi (ambayo sasa ni Wizara ya Elimu) na Serikali ya Manispaa Shanghai, chuo hiki kilifanywa moja ya vyuo vikuu na vyuo vya taaluma vya kwanza nchini China kuwa na mpango wa karo ambapo kwa pamoja unahusisha udhamini na mikopo ya wanafunzi.

1994-Sasa

Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai - SISU

kwa idhini ya Tume ya Elimu ya Serikali mwaka 1994, chuo kwa mara nyingine kilipata jina rasmi jina la Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (Shanghai International Studies University - SISU) na kuorodheshwa kama mojawapo ya vyuo vikuu vya kwanza kusimamiwa kwa ushirikiano kati ya Tume ya Elimu ya Nchi na Manispaa ya Shanghai. Mnamo 1996, SISU ilipita tathmini ya "Mradi wa 211" ulioongozwa na Tume ya Elimu ya Nchi, na ikawa mojawapo ya "vyuo vikuu 100 muhimu vya karne ya 21".

Tawi jipya lilijengwa mwaka 2000 lililo Songjiang, katika sehemu ijulikanayo kama “Mji wa Vyuo wa Songjiang - Songjiang University Town” Shanghai. Wanafunzi wote wa shahada ya kwanza na kisha wale wa uzamili walihamishiwa Songjiang. Tawi letu la Songjiang linajivunia majengo yake yenye miundo ya kimataifa na kwa hakika ni msingi unaokuza vipawa bora vya kimataifa.

Mwezi wa kwanza 2007, wito wa "Uadilifu, uaminifu, maono ya hekima na elimu pana (格高志远学贯中外)", ambao ni wito mpya mkuu wa SISU ulifumbuliwa. Huu ni wito ambao unaonyesha kina cha utendaji wa SISU.

Katika kipindi cha miaka 70 kufikia sasa, SISU imekua kutoka shule ya Kirusi yenye mkondo mmoja tu wa kitaaluma, ikawa chuo kikuu cha lugha za kigeni na sasa inazidi kuwa chuo kikuu cha fahari cha kimataifa. SISU imewahi kuikuzia nchi wataalamu wenye vipaji chungu nzima vya taaluma ambao wamehudumu kwa ustadi duniani kote wakichangia pakubwa katika maendeleo kiuchumi, kijamii na kukuza mawasiliano ya kirafiki na watu duniani kote.

Gawanya: