Press Contact

SISU News Center, Office of Communications and Public Affairs

Tel : +86 (21) 3537 2378

Baruapepe : news@shisu.edu.cn

Anuani :550 Dalian Road (W), Shanghai 200083, China

Soma Zaidi

Harakati za Rais Samia


28 September 2021 | By 褚予钦 Jamila | SISU

 

I. Utangulizi wa Kuingia Madarakani kwa Rais Samia

Samia Suluhu Hassan ndiye rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania. Alichukua wadhifa huo kufuatia kifo cha mtangulizi wake Dkt. John Magufuli mnamo Machi 17, mwaka huu. Rais Magufuli alifariki kutokana na maradhi ya moyo wakati alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. Hii ni mara ya kwanza kwa Watanzania kuzika rais aliyefariki akiwa madarakani katika miaka 60 ya Uhuru. (Kifo cha Magufuli: Hayati John Magufuli azikwa Chato, 2021) Kulingana na Katiba ya Tanzania, Rais Samia ataendelea kuwa rais wa nchi hadi mwaka 2025, yaani mwisho wa kipindi cha serikali ya sasa.

Mama Samia pia alikuwa makamu wa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania, kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kisiasa. Mnamo mwaka 2000-2005, alikuwa Waziri wa Ajira kwa Vijana, Maendeleo ya Wanawake na Watoto huko Zanzibar, na miaka mitano baadaye akawa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji huko Zanzibar. Alikuwa mbunge wa jimbo la Makunduchi visiwani Zanzibar kuanzia 2010 hadi 2015, na pia alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Mambo ya Muungano katika muda huo. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, alichukua fomu pamoja na Rais Magufuli na akachaguliwa kuwa makamu wa rais.

 

II. Harakati Muhimu za Rais Samia Baada ya Kushika Wadhifa

Kwa mujibu wa habari zilizotolewa na Rais Samia mwenyewe kwenye mitandao ya kijamii, (Hassan, 2021) harakati zake baada ya kuchukua urais ni kama ifuatavyo:

Machi 18, alitangaza rasmi taarifa ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli.

Machi 28, alipokea taarifa za mwaka wa Fedha 2019/2020 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). 

Aprili 11, alifanya safari yake ya kwanza kama Rais nchini Uganda na Rais Yoweri Museveni akielezea kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na kumaliza makubaliano ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka nchini Uganda. Uganda na Tanzania zilisaini mikataba mitatu yenye nia ya kuendeleza sekta ya mafuta na gesi ya Uganda, wakati wa ziara ya hiyo. (Rais wa Tanzania Samia Suluhu kufanya ziara ya kikazi nchini Kenya, 2021)

Aprili 12, alifanya mazungumzo na Rais mstaafu wa awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi. Walizungumza kuhusu jinsi ya kudumisha umoja na mshikamano nchini.

Aprili 19, alishiriki katika Kongamano la Viongozi wa Dini kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa maisha ya Hayati Dkt. John Magufuli pamoja na kuliombea Taifa.

Aprili 20, alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Mara Warwick kuhakikishia kuwa Benki ya Dunia itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Tanzania katika kukuza uchumi na kuinua ustawi wa wananchi.

Aprili 21, alikutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China wanaofanya biashara nchini Tanzania kujadili ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji katika nyanja mbalimbali. 

Aprili 23, alihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kueleza mwelekeo na vipaumbele vya Serikali ya awamu ya Sita, huku akisisitiza umuhimu wa uadilifu na kujitoa kwa ajili ya Taifa.

Aprili 30, katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alichaguliwa kwa kura zote kuwa Mwenyekiti. Hivyo, akawa mwenyekiti wa kwanza mwanamke wa CCM katika historia ya chama hicho tawala.

Kuanzia tarehe 4 hadi 6, Mei, alifanya ziara rasmi ya kikazi nchini Kenya. Alikutana na Mhe. Rais Uhuru Kenyatta, na viongozi hawa wawili wamekubaliana kuondoa vikwazo vya biashara na kufungua milango zaidi ya watu kuwekeza kwa ajili ya kuinua uchumi.

Mei 24, alishiriki katika mkutano wa Mtandao wa Viongozi Wanawake Barani Afrika (African Women Leaders Network), na alieleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuwaletea Watanzania maendeleo.

Mei 28, alikutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN-Women) Dkt. Phumzile Mlambo-Ngcuka. Siku ile, alishiriki katika Mkutano wa Masuala ya Kijinsia na akakubali kuwa kiongozi katika eneo la haki za kiuchumi. Pia aliahidi kuwa, serikali yake itaendelea kusimamia misingi ya usawa wa kijinsia ili kuhakikisha tunafikia kiwango cha 50/50 katika uongozi.

Kuanzia tarehe 13 hadi 15, Juni, alifanya ziara ya siku tatu mkoani Mwanza, ambao uko Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania, karibu na Ziwa Viktoria. Katika ziara hii, alikagua ujenzi wa Daraja la JPM, Reli ya Kisasa (SGR) Mwanza-Isaka na Meli ya MV Mwanza, na pia alishudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi na ukarabati wa meli nyingine tano.

 

III. Uchambuzi wa Sera za Rais Samia

Baada ya Mama Samia achukue urais, kulitokea maoni mengi tofauti juu ya mwelekeo wa sera za rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania. 

Baadhi ya watu wanaamini kuwa serikali yake ya awamu ya sita italeta matumaini ya mabadiliko ya sera kwa Tanzania. Kampuni za kigeni zinatumai kuwa Rais Samia atabadilisha sera kali za Rais Magufuli kwao, hasa kwa kampuni za madini. Wawekezaji wageni wanatumai vizuizi vya visa vitapunguzwa na mazingira ya biashara yataboreshwa. Vyama vya upinzani vinatumai kuwa rais huyu mpya anaweza kulegeza ukandamizaji na kuwapa uhuru zaidi.

Kwa upande mwingine, kuna sauti kadhaa zinazoamini kuwa itakuwa ngumu kwa Rais Samia kuweka ushawishi mkubwa. Chama cha Mapinduzi (CCM) ina utamaduni wa vikundi tofauti na mapigano makali. Kwa sasa, kuna “Kikundi cha Magufuli” na “Kikundi cha Kikwete” ndani yake. (殷悦, 2021) Kwa kipindi cha muda, Samia atakumbwa na matatizo ya ndani ya chama, na ni ngumu kwake kufanya mageuzi ya kimsingi. Itambidi Samia atumie busara yake ya kisiasa ili kuwaunga wanachama wenye maoni tofauti. Lakini, kwa sababu ya utambulisho wake wa Mzanzibari na Mwislamu, atakuwa na shida kupata tegemezo katika eneo la Kikristo barani, kwa hivyo ni ngumu kwake kuweka ushawishi mkubwa juu ya hali ya kisiasa.

i. Upangaji Mpya wa Serikali

Zaidi ya harakati zilizotajwa hapo juu, kitendo kingine muhimu cha Rais Samia kilikuwa upangaji wake mpya wa kisiasa wa ndani, ikiwemo upangaji wa mawaziri wa serikali na wakuu wa mikoa. Yasemekana kwamba, mabadiliko hayo yanafanana kwa kiasi kikubwa, yaani kwa kimsingi aliwahamisha mawaziri kutoka wizara au mkoa moja kwenda nyingine. 

Katika mchakato wa kupanga upya wakuu wa mikoa, Rais Samia alifanya vizuri katika kusawazisha vikosi. Katika orodha mpya iliyotangazwa na Ikulu Mei 15 mwaka huu, katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, wakuu wa mikoa tisa tu wameondolewa, kustaafu au kupangiwa majukumu mengine lakini theluthi mbili ya waliokuwepo wamebaki. (Uteuzi wa Wakuu wa Mikoa: Nini maana ya uteuzi wa wakuu wa mikoa uliofanywa na Rais Samia?, 2021) 

Kwa mfano, uteuzi wa Queen Sendiga kutoka chama cha upinzani cha ADC kuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa umetoa tafsiri kwamba Rais Samia ametimiza ahadi yake kuwa kwenye kuteua hataangalia chama kimoja tu cha siasa. Uteuzi wa wakuu wa Mtwara na Ruvuma ambayo ni mikoa inayopakana na Msumbiji umeendeleza utamaduni wa kutumia wanajeshi kuwa wakuu wa mikoa yenye changamoto za kiusalama. Na uteuzi wa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam umetoa matumaini mapya kwa baadhi ya wanachama wa CCM ambao walijisikia kama wametengwa wakati wa utawala wa Magufuli.

ii. Mwelekeo Mpya kwa Virusi vya Korona

Baada ya kushika wadhifa, Rais Samia hakutumia muda mrefu kutoa uamuzi wa kuunda kamati iliyopewa jukumu la kushughulikia COVID-19 na chanjo kutoka kwa kituo cha COVAX kwa nchi zinazoendelea, ambao uilionyesha mabadiliko kamili kutoka kwa utawala uliopita. (Tanzania: President Samia Suluhu Hassan's 100 days in office, 2021)

Katika hotuba zake nyingi na hata habari alizotumia kwenye mitandao ya kijamii, Rais Samia amewasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 na kufuatana na maelezo ya wataalamu wa afya. Kama vile, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kutogusana. Amesisitiza mara kwa mara kwamba ugonjwa wa Korona upo.

Zaidi ya hayo, yeye pia ameonyesha hamu kubwa ya kushirikiana kikamilifu na jamii ya kimataifa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Kwa mfano, katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken, walijadili kuhusu ushirikiano wa Marekani na Tanzania katika maswali kadhaa yakiwemo mapambano dhidi ya janga la virusi vya korona. (Marekani yaahidi kushirikiana na Tanzania kwenye janga la corona, 2021)

iii. Ishara Mpya katika Mambo ya Nje

Rais Samia pia amekuwa na nia ya kuboresha taswira ya Tanzania kimataifa. Yasemekana kwamba, kitendo chake cha kuchagua Liberata Mulamula, ambaye alikuwa balozi wa zamani wa Marekani kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kimeonyesha nia yake ya kuweka ishara nzuri ya kuboresha uhusiano wa kimataifa. 

Baada ya kushika wadhifa, Rais Samia amesafiri kwenda Uganda mara mbili na pia alifanya ziara rasmi ya siku mbili nchini Kenya. Wakati alipokuwa nchini Uganda, Rais Samia na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wa wamesaini rasmi mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kujenga bomba la mafuta ghafi kutoka Magharibi mwa Uganda hadi bandari ya Tanga Tanzania. (Uganda na Tanzania zasaini mkataba ujenzi wa bomba la mafuta, 2021) Wakati alipokuwa nchini Kenya, rais huyu mpya wa Tanzania alitafuta fursa za kurekebisha uhusiano na Kenya, ambao ulikuwa umeharibika kidogo chini ya uongozi wa Magufuli, kwa kuwa nchi hizo mbili zilikuwa na mizozo juu ya biashara ya kuvuka mpaka, ushuru na zinginezo. (Rais wa Tanzania Samia Suluhu kufanya ziara ya kikazi nchini Kenya, 2021)

 

IV. Ujumla na Utabiri

Kwa jumla, Rais Samia ni mwanasiasa yenye tamaa na imani. Siku za baadaye ataendelea vitendo vyake vya kuziba pengo kati ya vikundi tofauti katika chama tawala, kama alivyosema katika hotuba yake ya kuapishwa kuwa alitarajia kufikia makubaliano kupitia majadiliano ya wote. Na pia inaaminika kwamba serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake itaendelea kuboresha uhusiano wa kimataifa wa Tanzania. 

Ikumbukwe kwamba kama rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania na hata Afrika ya Mashariki, ulimwengu wa nje utazingatia zaidi hatua za Rais Samia juu ya maswala ya wanawake. Lakini, maisha yake ya kisiasa hayakumtambulisha kama  mwanaharakati wa masuala ya wanawake. Kwa hivyo, umuhimu ni kwamba ameahidi kushughulikia usawa wa kijinsia na maswala mengine husika katika siasa.

Gawanya:

Press Contact

SISU News Center, Office of Communications and Public Affairs

Tel : +86 (21) 3537 2378

Baruapepe : news@shisu.edu.cn

Anuani :550 Dalian Road (W), Shanghai 200083, China

Soma Zaidi